Katika kutekeleza majukumu yake ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa bandari, Chuo cha Bandari kinaendesha mafunzo ya "Port operations" kwa wafanyakazi wa kurugenzi za Sheria na Ulinzi. Mafunzo mengine ni "Port Pricing and Tariff na "Terminal and Yard Planning" yanayofanyika kwa wafanyakazi wa Idara ya Utekelezaji.
Mafunzo haya yamefunguliwa rasmi leo tarehe 23 Septemba 2024 na Mkuu wa Chuo cha Bandari Dr. Lufunyo Hussein na yatafanyika kwa muda wa siku tano.
Katika Ufunguzi huo, Dr. Lufunyo aliwaelezea wafanyakazi mwelekeo wa taasisi katika eneo la kuwajengea uwezo wafanyakazi wake.
Dr. Lufunyo alisema lengo la chuo ni kuhakikisha kila mtumishi anajua kazi za msingi zinazofanywa na Taasisi ili wafanyakazi wote wawe na uelewa wa pamoja wa kazi na huduma zinazotolewa na Mamlaka. Hivyo Chuo kina jukumu la kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kila idara ili kufikia malengo ya taasisi.
‘’Kila mtumishi kutoka kila idara anapaswa kufahamu kazi za msingi za taasisi ili aweze kutoa huduma nzuri kwa wateja, hivyo chuo cha bandari kina jukumu la kuhakikisha watumishi wanajengewa uwezo kwa njia ya mafunzo yanayotolewa hapa chuoni’’.
Naye mkurugenzi wa huduma za sheria, Bw. Stanslaus Kagisa ametoa shukrani kwaniaba ya washiriki wa mafunzo hayo huku akikipongeza chuo kwa namna kinavyotekeleza sera ya mafunzo ya Mamlaka kwa watumishi wote. Pia amepongeza uongozi wa chuo kwa jitihada zake kwenye kupambanua fursa zilizopo katika sekta ya bandari na uchukuzi kwa ujumla kwa kutengeneza mitaala inayoendana na madiliko ya kila siku kwa kutoa mchango katika uchumi wa buluu.
Chuo kinaendela kutoa kozi za muda mfupi pamoja na ushauri wa kitaalamu katika taasisi za serikali na za binafsi, chuo kina wakaribisha wadau wote kujiunga katika kozi zitolewazo na chuo.